Enendeni na alikeni kila mtu kwenye Karamu (Rej. Mt. 22:9)

Ndugu wapendwa!

Mada niliyochagua kwa ajili ya Siku ya Misioni Duniani ya mwaka huu inatoka katika mfano wa Injili kuhusu Karamu ya Arusi (Mt 22: 1-14). Baada ya wageni kukataa mwaliko wake, mfalme, mhusika mkuu katika simulizi, anawaambia watumishi wake: “Basi, enendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini” (Mt 22:9). Tukitafakari kifungu hiki muhimu katika muktadha wa mfano na maisha ya Yesu mwenyewe, tunaweza kutambua vipengele kadhaa muhimu vya uinjilishaji. Hivi vinaonekana ni muafaka kwetu sote, kama wafuasi wamisionari wa Kristo, katika hatua hii ya mwisho ya safari ya sinodi ambayo, kadiri ya kauli mbiu yake, “Ushirika, Ushiriki na Umisionari” inalenga kulielekeza Kanisa upya katika kazi yake ya msingi, ambayo ni kuhubiri Injili katika ulimwengu wa leo.

  1. “Enendeni na alikeni” Utume kama kutoka kusikochosha kwenda kuwaalika wengine kwenye karamu ya Bwana.

Katika amri ya mfalme kwa watumishi wake tunapata maneno mawili yanayoelezea moyo wa utume: kitenzi “kutoka” na “kualika”.

Kama ilivyo kwa ya kwanza, tunapaswa kukumbuka kwamba watumishi walikuwa wametumwa hapo awali kupeleka mwaliko wa mfalme kwa wageni (Mt 22:3-4). Utume, tunaona, ni kwenda bila kuchoka kwa wanaume na wanawake wote, ili kuwaalika kukutana na Mungu na kuingia katika ushirika naye. Bila kuchoka! Mungu, mkuu katika upendo na mwingi wa huruma, mara   kwa mara anaondoka ili kukutana na wanaume na wanawake wote, na kuwaita kwenye furaha ya ufalme wake, hata katika hali ya kutojali au kukataa kwao. Yesu Kristo, Mchungaji Mwema na mjumbe wa Baba, alitoka kwenda kuwatafuta kondoo waliopotea wa watu wa Israeli na akatamani kwenda mbali zaidi, kwa ajili ya kuwafikia hata kondoo wa mbali zaidi. (Yn 10:16). Kabla na baada ya kufufuka kwake, aliwaambia wanafunzi wake “Nendeni”, hivyo kuwahusisha katika utume wake mwenyewe (Lk 10:3; Mk 16:15). Kanisa, kwa upande wake, katika uaminifu katika utume lilioupokea kutoka kwa Bwana, litaendelea kwenda hadi miisho ya dunia, kuanza safari tena na tena, bila kuchoka kamwe wala kukata tamaa mbele ya magumu na vikwazo.

Ninachukua fursa hii kuwashukuru wale wamisionari wote ambao, kwa kuitikia wito wa Kristo, wameacha kila kitu nyuma kwenda mbali na nchi yao ya asili na kuleta Habari Njema mahali ambapo watu bado hawajaipokea, au wameipokea hivi majuzi tu. Wapendwa, kujitolea kwenu kwa ukarimu ni kielelezo dhahiri cha kujitoa kwenu kwa utume ad gentes ambao Yesu aliwakabidhi wanafunzi wake: “Enendeni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi” (Mt 28:19). Tunaendelea kusali na tunamshukuru Mungu kwa miito mipya na mingi ya kimisionari kwa ajili ya kazi ya uinjilishaji hadi miisho ya dunia.

Tusisahau kwamba kila Mkristo ameitwa kushiriki katika utume huu wa kiulimwengu, kwa kutoa ushuhuda wake mwenyewe kwa Injili katika kila muktadha, ili Kanisa lote liweze kuendelea mbele na Bwana na Mwalimu wake hadi njia panda za dunia ya leo. “Changamoto ya leo katika Kanisa ni kwamba, Yesu anaendelea kugonga mlango, lakini kutoka ndani, ili tumruhusu atoke! Mara nyingi tunaishia kuwa Kanisa la ‘kifungo’ ambalo halimruhusu Bwana atoke nje, ambalo linamweka kama ‘mali yake’ ilihali, Bwana alikuja kwa ajili ya utume na anatutaka tuwe wamisionari” (Hotuba kwa Washiriki katika Kongamano lililoandaliwa na Dikasteri ya Walei, Familia na Maisha, 18 Februari 2023). Sisi sote tuliobatizwa, na tuwe tayari kuondoka upya, kila mmoja kadiri ya hali yake ya maisha, kuanzisha vuguvugu jipya la kimisionari, kama vile wakati wa mapambazuko ya Ukristo!

Tukirejea katika amri ya mfalme katika mfano huo, watumishi wanaambiwa sio tu “kwenda”, lakini pia “kualika”: “Njoni Arusini!” (Mt 22:4). Hapa tunaweza kuona kipengele kingine, japo si kidogo kwa umuhimu, cha utume toka kwa Mungu. Kama tunavyoweza kufikiria, watumishi waliwasilisha mwaliko wa mfalme kwa uharaka lakini pia kwa heshima kubwa na wema. Vivyo hivyo, utume wa kuleta Injili kwa kila kiumbe lazima uige “mtindo” ule ule wa Yule anayehubiriwa. Katika kuutangazia ulimwengu “uzuri wa upendo wa wokovu wa Mungu uliodhihirishwa katika Yesu Kristo ambaye alikufa na kufufuka kutoka kwa wafu” (Evangelii Gaudium, 36), wanafunzi wamisionari wanapaswa kufanya hivyo kwa furaha, ukuu na ukarimu, ambayo ni matunda ya Roho Mtakatifu ndani yao (Rej. Gal 5:22). Si kwa kushinikiza, kulazimisha au kugeuza watu imani, bali kwa ukaribu, huruma na upole, kwa njia hii kuakisi namna ya Mungu ya kuwa na kutenda.

  1. “Kwenda Arusini “. Mwelekeo wa kieskatolojia na Kiekaristi wa Utume wa Kristo na Kanisa

Katika mfano huo, mfalme anawaomba watumishi kupeleka mwaliko kwajili ya Arusi ya mwanae. Karamu hiyo ikiwa ni kiashiria cha Karamu ya kieskatolojia. Ni taswira ya wokovu wa mwisho katika Ufalme wa Mungu, unaotimizwa hata sasa kwa kuja kwa Yesu, Masiha na Mwana wa Mungu, ambaye ametupa uzima tele (Yn 10:10), unaofananishwa na meza iliyowekwa pamoja na vyakula vitamu na kwa divai nzuri, wakati Mungu atapoharibu kifo milele (Isa 25:6-8).

Utume wa Kristo unahusiana na utimilifu wa wakati, kama alivyotangaza mwanzoni mwa mahubiri yake: “Wakati umetimia, na Ufalme wa Mungu umekaribia” (Mk 1:15). Wafuasi wa Kristo wanaitwa kuendeleza utume huu wa Bwana na Mwalimu wao. Hapa tunafikiria fundisho la Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikani juu ya tabia ya kieskatologia ya msukumo wa kimisionari wa Kanisa: “Wakati wa kazi ya kimisionari unaendelea kati ya ujio wa kwanza wa Bwana na wa pili…, kwa maana Injili lazima ihubiriwe kwa mataifa yote, kabla ya Bwana kuja (Rej. Mk 13:10)” (Ad Gentes, 9).

Tunajua kwamba miongoni mwa Wakristo wa kwanza bidii ya umisionari ilikuwa na mwelekeo wenye nguvu wa kieskatolojia. Waliona uharaka wa kuhubiriwa kwa Injili. Leo pia ni muhimu kudumisha mtazamo huu, kwa kuwa inatusaidia kueneza injili kwa furaha ya wale wanaojua kwamba “Bwana yu karibu” na kwa tumaini la wale wanaosonga mbele kuelekea lengo, wakati sisi sote tutakuwa pamoja na Kristo kwenye karamu yake ya arusi katika ufalme wa Mungu. Wakati ulimwengu unaweka mbele yetu “karamu” mbalimbali za ulaji, kujistarehesha, kujilimbikizia mali na ubinafsi, Injili inamualika kila mtu kwenye karamu ya kimungu, inayopambwa na furaha, ushirikiano, haki na udugu katika ushirika na Mungu na wengine.

Utimilifu wa maisha, ambayo ni zawadi ya Kristo, unatarajiwa hata sasa katika karamu ya Ekaristi, ambayo Kanisa huadhimisha kwa amri ya Bwana kwa kumbukumbu yake. Mwaliko wa karamu ya kieskatolojia tunaotoa kwa kila mtu katika utume wetu wa uinjilishaji unahusishwa kwa kiasi kikubwa na mwaliko kwa meza ya Ekaristi, ambapo Bwana hutulisha kwa Neno lake na kwa Mwili na Damu yake. Kama vile Benedikto XVI alivyofundisha: “Kila adhimisho la Ekaristi linatimiza kisakramenti mkusanyiko wa kieskatolojia wa watu wa Mungu. Kwetu sisi, karamu ya Ekaristi ni mwonjo wa kweli wa awali wa karamu ya mwisho iliyotabiriwa na manabii (Rej. Isa 25: 6-9) na kuelezewa na Agano Jipya kama ‘arusi ya mwanakondoo’ (Ufu. 19:9), itakayoadhimishwa katika furaha ya ushirika wa watakatifu” (Sacramentum Caritatis, 31).

Kwa hiyo, sisi sote tunaitwa kushuhudia kwa uthabiti zaidi kila Adhimisho la Ekaristi, katika nyanja zake zote, na hasa mwelekeo wake wa kieskatolojia na kimisionari. Katika msingi huu, ningerudia kusema kwamba, “Hatuwezi kukaribia meza ya Ekaristi bila kuvutwa katika utume ambao, kwa kuanzia moyoni kabisa mwa Mungu, unakusudiwa kuwafikia watu wote” (Rej. aya 81). Upyaisho wa Ekaristi Takatifu ambao Makanisa mengi mahalia yanautangaza kwa bidii katika enzi ya baada ya UVIKO-19 pia itakuwa muhimu kwa ajili ya kufufua roho ya kimisionari katika kila muamini. Kwa imani kubwa kiasi gani na shauku ya kutoka moyoni tunapaswa kutamka katika kila Misa: “Tunatangaza kifo chako, Ee Bwana, na kutukuza Ufufuko wako, mpaka utakapokuja tena”!

Katika mwaka huu uliotengwa kwa ajili ya sala kwa ajili ya maandalizi ya Jubilei ya 2025, napenda kuwahimiza wote wazidishe majitoleo yao na zaidi sana kushiriki katika maadhimisho ya Misa na kusali kwa ajili ya utume wa Kanisa wa Uinjilishaji. Kwa kulitii agizo la Mwokozi, haliachi kusali, katika kila adhimisho la Ekaristi na liturujia, “Baba Yetu”, kwa kuomba, “Ufalme wako ufike”. Kwa njia hii, sala ya kila siku na Ekaristi kwa namna ya pekee vinatufanya kuwa mahujaji na wamisionari wa matumaini, tukisafiri kuelekea uzima wa milele ndani ya Mungu, kuelekea karamu ya Arusi ambayo Mungu amewaandalia watoto wake wote.

  1. “Kila mtu”. Utume wa kiulimwengu wa wafuasi wa Kristo katika Kanisa la kisinodi na la kimisionari katika ukamilifu wake

Tafakari ya tatu na ya mwisho inahusu wapokeaji wa mwaliko wa mfalme: “kila mtu”. Kama nilivyosisitiza, “Huu ndio moyo wa utume: kwamba “wote”, bila kumuacha mtu yeyote. Kila utume wetu, basi, huzaliwa kutoka kwa moyo wa Kristo ili aweze kuwavuta wote kwake” (Hotuba kwa Mkutano Mkuu wa Mashirika Kipapa ya Kimissionari, 3 Juni 2023). Leo, katika ulimwengu uliosambaratishwa na migawanyiko na migogoro, Injili ya Kristo inabakia kuwa sauti ya upole lakini thabiti inayowaita watu binafsi kukutana, kutambua kwamba wao ni kaka na dada, na kufurahi katika utulivu katikati ya tofauti. “Mungu Mwokozi wetu anatamani kila mtu aokolewe na kupata kuujua ukweli” (1Tim 2:4) Basi, tusisahau kamwe kwamba katika shughuli zetu za umisionari tunaombwa kuhubiri Injili kwa watu wote: “Badala ya kuonekana waziwazi kulazimisha majukumu mapya, {sisi} tunapaswa kuonekana kama watu wanaotaka kushirikisha furaha yao, wanaoelekeza kwenye upeo wa uzuri na wanaowaalika wengine kwenye karamu nono” (Evangelii Gaudium, 14).

Wafuasi wamisionari wa Kristo sikuzote wamekuwa wakiguswa kutoka moyoni kwa ajili ya watu wote, haidhuru hali yao ya kijamii au hata kimaadili. Mfano wa Arusi unatuambia kwamba, kwa amri za mfalme, watumishi walikusanyika, “wote waliowaona, wema na wabaya” (Mt 22:10). Zaidi ya hayo, “maskini, viwete, vipofu na viwete” (Lk 14:21), kwa neno moja, kaka na dada zetu walio wadogo kabisa, wale waliotengwa na jamii, ndio wageni maalum wa mfalme.​ Karamu ya arusi ya mwanawe ambayo Mungu ametayarisha inabaki wazi kila wakati kwa wote, kwa kuwa upendo wake kwa kila mmoja wetu ni mkubwa na hauna masharti. “Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” (Yoh 3:16). Kila mtu, kila mwanamume na kila mwanamke, anaalikwa na Mungu kushiriki neema yake, ambayo inabadilisha na kuokoa. Mtu anahitaji tu kusema “ndiyo” kwa zawadi hii ya kimungu isiyo na malipo, akiikubali na kujiruhusu kugeuzwa nayo, na kuivaa kama “joho la arusi” (Rej. Mt 22:12).

Umisionari kwa wote unahitaji uwajibikaji wa wote. Tunahitaji kuendelea na safari yetu kuelekea Kanisa kamili la kisinodi na kimisionari katika huduma ya Injili. Hulka ya Kisinodi (Synodality) kimsingi ni ya kimisionari na, kinyume chake, umisionari daima una hulka ya ki-sinodi. Kwa hiyo, ushirikiano wa karibu wa kimisionari leo ni wa muhimu sana na wa lazima zaidi, katika Kanisa la kiulimwengu na katika Makanisa Mahalia. Katika nyayo za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikani na Watangulizi wangu, napendekeza kwa majimbo yote duniani huduma ya Mashirika Kipapa ya Kimissionari. Yanawakilisha nyenzo ya msingi “ambayo kwayo wakatoliki wanalelewa kutoka utotoni kwa mtazamo wa kweli wa kiulimwengu na wa kimisionari na {ni} njia pia ya kuanzisha ukusanyaji mzuri wa fedha kwa ajili ya misioni zote, kila moja kulingana na mahitaji yake (Ad Gentes, 38). Kwa sababu hiyo, michango ya Siku ya Misioni Ulimwenguni katika Makanisa yote mahalia imekusudiwa kwa ukamilifu kwa ajili ya mfuko wa kiulimwengu wa mshikamano ambao Shirika la Kipapa la Uenezaji wa Imani kisha linagawanya kwa jina la Papa kwa ajili ya mahitaji ya utume wote wa Kanisa. Tuombe kwamba Bwana atuongoze na atusaidie kuwa zaidi Kanisa la kisinodi na la kimisionari (Rej. Homilia kwa ajili ya Misa ya Kuhitimisha Mkutano Mkuu wa Kawaida wa Sinodi ya Maaskofu, 29 Oktoba 2023).

Hatimaye, hebu tuinue macho yetu kwa Maria, ambaye alimwomba Yesu afanye muujiza wake wa kwanza tena arusini, huko Kana ya Galilaya (Rej. Yn 2:1-12). Bwana alitoa kwa maarusi wapya na wageni wote divai mpya ya kutosha, kama kielelezo cha karamu ya arusi ambayo Mungu anatayarisha kwa wote mwishoni mwa wakati. Hebu tuombe maombezi yake ya kimama kwa ajili ya utume wa kueneza Injili kwa wafuasi wa Kristo katika nyakati zetu hizi. Kwa furaha na upendo wa mama yetu, kwa nguvu inayotokana na huruma na upendo (Rej. Evangelii Gaudium, 288), tusonge mbele kumpelekea kila mtu mwaliko wa Mfalme, Mwokozi wetu. Maria Mtakatifu, Nyota ya Uinjilishaji, utuombee!

Roma, Mtakatifu Yohane Laterano, 25 Januari 2024, Sikukuu ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo

FRANSISKO